Michezo

Taifa Stars yapewa ushauri AFCON 2019

0
Taifa Stars AFCON 2019
Taifa Stars

Baada ya kuteguliwa kwa kitendawili cha makundi na ratiba ya fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2019), ambako Tanzania imepangwa Kundi C, sambamba na Senegal, Algeria na Kenya, wadau wa soka wametoa maoni yao, huku wakisisitiza hakuna kinachoshindikana.

Droo ya makundi na ratiba ya AFCON 2019, fainali zitakazofanyika nchini Misri Juni hadi Julai mwaka huu, ilipangwa juzi jijini Cairo, ambako macho na masikio ya Watanzania yalielekezwa huko kujua wapin-zani wa fainali hizo za kwanza baada ya miaka 39.

Hafla hiyo ambayo ilihudhuriwa na wajumbe kutoka Tanzania, wakiongozwa na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, pamoja na Kocha Mkuu wa timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Emmanuel Ammunike, ilishuhudiwa dunia nzima kupitia vituo vya runinga.

Nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Morocco, Mustapha Hadj, alikuwa ni mmoja wa waliohudhuria hafla hiyo, kama ilivyokuwa pia kwa El Hadji Diouf, nyota wa zamani wa Liverpool na timu ya Taifa ya Senegal, nahodha wa zamani wa Misri, Ahmed Hassan, Yaya Toure na wengineo wengi.

Soma pia:  Serengeti Boys dhidi ya Nigeria AFCON U-17

Kundi A lina nchi za Misri, Zimbabwe, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), huku kundi B likiwa na nchi za Burundi, Madagascar, Guinea na Nigeria, wakati Kundi C lina nchi za Tanzania, Kenya, Algeria na Senegal.

Kundi D lina nchi za Afrika Kusini, Namibia, Ivory Coast na Morocco, wakati Kundi E lina nchi za Angola, Mauritania, Mali na Tunisia, huku Kundi F likiwa na nchi za Guinea Bissau, Benin, Ghana na Cameroon.

Akizungumza jana, Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Mexime, ameizungumzia droo na kundi C kwa ujumla na kusema kwamba kikubwa ambacho kitafanikisha kushiriki mwema michuano hiyo ni maandalizi bora na si vinginevyo.

Mexime alisema haoni cha ajabu katika kundi hilo, kwani ndizo timu ambazo wanatakiwa kukutana nazo, hivyo hakuna ujanja mwingine zaidi ya kupambana na wapinzani ambao Tanzania imepangwa nao kundi moja.

Soma pia:  Benpol amvisha pete mchumba wake Arnelisa

“Hatutakiwi kuangalia tumepangwa na nani, tunachotakiwa ni kupambana vilivyo na tusonge mbele zaidi, kwani hao ndio tuliopangwa nao, hakuna kuogopa,” alisema Mexime.

Naye Kocha Msaidizi wa African Lyon, Salvatory Edward, alisema kundi hilo lina tafsiri mbili, unaweza kusema ni gumu na rahisi, kwa sababu wapinzani wa Taifa Stars, ambao ni Senegal na Algeria, wana idadi kubwa ya wachezaji nje ya Afrika, huku Kenya wakifahamiana kwa kiasi kikubwa.

Edward ambaye pia aliwahi kucheza Taifa Stars na Yanga, na baadaye kuwa Kocha Msaidizi wa Yanga, alisema pamoja na Algeria na Senegal kuwa na idadi kubwa ya wachezaji nje ya Afrika, lakini hata Stars ina idadi kubwa ya wachezaji nje ya nchi.

Aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, Malota Soma ‘Ball Jaggler’ alisema timu zote zilizotinga katika michuano hiyo hazikuingia kwa bahati mbaya, hivyo kilichopo ni maandalizi ya aina yake ambayo yatasaidia timu hiyo kufanya vizuri.

Ball Jaggler alisema kocha Amunike anatakiwa kuwekea mkazo eneo la ushambuliaji, kwani washambuliaji wetu wanakosa umakini jambo ambalo linasababisha mdororo wa mabao jambo ambalo linakwamisha maendeleo ya timu zetu.

Soma pia:  TP - Mazembe yahitimisha safari ya Simba CAF Champion League

Alitolea mfano wa mechi ya kwanza ya Simba dhidi ya TP Mazembe, iliyochezwa uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, timu hiyo ilikosa mabao mengi ya wazi ambayo jana yangeisaidia timu hiyo na kusonga mbele katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL).

Aidha, Taifa Stars imefuzu fainali hizo zitakazofanyika Juni 21 hadi Julai 19, baada ya kumaliza nafasi ya pili nyuma ya Uganda, ilikojikusanyia pointi nane, zilizotokana na ushindi katika mechi mbili na sare mbili, katika Kundi L ilikofungwa pia mechi mbili.

Vinara na washindi wa pili wa makundi sita yenye timu nne nne, watafuzu hatua ya mtoano ‘play off ’ ya 16 Bora, sambamba na mataifa manne yatakayomaliza katika nafasi za tatu zikiwa na matokeo bora ‘best looser.’

Comments

Comments are closed.

More in Michezo