Makala

Kamari inavyoliza maelfu na kumchekesha mmoja

0

Hivi karibuni nchi yetu imeingiliwa na utamaduni mpya wa kamari kutoka nje. Tunaona jinsi vijana wetu wanavyotumbukia katika mtindo huu wa maisha, wakishawishiwa na matangazo ya redio na runinga.

Kamari hii imepewa jina la ‘kubeti’ na majina mengi mengi tu. Ni kamari inayotegemea mtandao au simu ya mkononi au ‘mkeka’. Hii imepamba moto na vijana wetu wameghumiwa na ndoto ya kupata ‘mshahara’ bure mwaka mzima bila ya kufanya kazi.

Wengine wanatangazwa kuwa wameshinda nyumba, wengine bodaboda, wengine mamilioni mkononi. Ili mradi vijana wetu wanaacha masomo na kazi na sasa wanakimbilia kamari.

Hasara za Kamari na Kubeti

Kamari

Hata kama kupitia kamari hiyo yapo makusanyo yanayoingia katika pato la nchi kupitia kodi, hapana siri vijana wetu wanazidi kuwehuka na kuacha masomo au kazi; wanakwenda pabaya kuliko uzuri mdogo unaoweza kuonekana na kutajwa.

Hata katika vikundi vya kazi kama teksi, bodaboda, biashara, shule na mambo mengine muhimu katika uzalishaji, ukuzaji uchumi na ujenzi wa jamii bora, kubeti kumeteka vijiwe na mijadala.

Eti hiyo sasa imebaki ndiyo kazi! Sasa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha imetangaza kuzuia ‘kwa muda’ matangazo yote ya michezo ya kubahatisha katika redio na runinga.

Bodi imesema matangazo hayo yamekuwa mengi kiasi cha ‘kuharibu taswira’ ya michezo hiyo. Bodi imezuia matangazo haya kwa muda usiojulikana.

Kimsingi, licha ya matangazo hayo kuwa mengi kiasi cha kuharibu taswira ya michezo hii, bado tatizo ni zaidi ya matangazo kuwa mengi; ni michezo hiyo kuendelea kuwa ni kamari inayoliza wengi kwa manufaa ya mmoja anayepata na kutangazwa ili kuhamasisha wengine.

Kwa mtazamo wangu, ninaunga mkono juhudi za serikali kudhibiti matangazo hayo, lakini ninashauri nguvu isiishie tu kudhibiti matangazo ya redio na runinga, bali pia hata yanayopitia katika ujumbe mfupi wa maandishi katika simu (SMS).

Bodi inasema wanatekeleza agizo la Rais John Magufuli kuhusu matangazo. Sina hakika iwapo Rais Magufuli na viongozi wa dini walizungumzia matangazo ya redio na TV tu, au walizungumzia kamari kama kamari.

Kamari na Dini

Waliposema dini zimeharamisha kamari hawakumaanisha zimeharamisha matangazo ya redio na TV tu. Hapa bodi inapaswa kufafanua vizuri na kuweka msimamo imara ili uamuzi wake huo mzuri utekelezwe kwa tija kwa manufaa ya jamii na taifa kwa jumla.

Itakumbukwa kuwa suala hili liliibuka wakati viongozi wa dini walipokutana na Rais Magufuli Ikulu, Dar es Salaam.

Soma pia:  Fahamu namna ya kukabili moto wa jikoni

Ndipo kiongozi mmoja aliposimama na kusema anashangazwa na tabia ya vyombo vya habari kufanya matangazo ya kamari licha ya kuwa ni haramu katika dini zote.

“Kwenye Biblia na Quran imeandikwa kamari ni haramu, lakini hapa Tanzania vijana wanacheza kamari kupitia mitandao. Ukifungua TV unakuta matangazo ya kamari. Haya makampuni wao ni hapa kamari tu. Hapa Tanzania michezo hii imeenea na kauli yako ya hapa kazi tu imekuwa hapa kamari tu,” alisema kiongozi huyo.

Kinachosikitisha ni kuona baadhi ya viongozi na baadhi ya watendaji katika baadhi ya vyombo vya serikali, wanashirikishwa na kutumiwa katika michezo hii inayochochea uvivu, badala ya kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kuinua uchumi kwa mtu mmoja mmoja, familia, vikundi na taifa kwa jumla.

Hawa, wanatumika kama wageni rasmi katika kutoa zawadi kwa washindi, hivyo nao wanakuwa wahamasishaji.

Kauli ya Rais Magufuli kuhusiana na Kamari

Rais akaongeza kusema mwishowe vijana wetu wanameza kasumba kuwa kamari inalipa mshahara wa bure wa mwaka mzima na kwa hiyo hakuna haja ya kufanya kazi za kujituma.

Rais akaitika kilio cha viongozi wa dini na akamuagiza Waziri Mkuu kushughulikia suala hili na kuchukua hatua stahiki.

Tukiangalia katika mtandao tunaona wananchi wengi wanakubaliana kabisa na hatua alizochukua Rais.

Wengine wanasema kamari inahamasisha uvivu tu, kwani mshahara unapaswa kuwa malipo ya kazi mtu anayofanya na si vinginevyo. Wengine wanasema sasa baada ya matangazo ya kamari kupigwa marufuku waache pia kutusumbua na SMS zao.

“Tumenunua simu kwa ajili ya mambo muhimu siyo tunasumbuliwa kwa SMS za matangazo ya biashara za kipuuzipuuzi. Wapige marufuku na hizi SMS za matangazo, kwani kama hawajapiga marufuku watahamia kwenye simu zetu,” anasema mwananchi mmoja.

Wapo wanaosema kamari ina faida kwani wengi wameishia kutajirika baada ya fedha chache walizowekeza.

Ukweli ni kuwa, hayo matangazo hutuambia tu kuhusu walioshinda, hawataji asilani walioshindwa na idadi ya mamilioni kama siyo mabilioni waliyopoteza wananchi hao huku kampuni husika za kamari zikivuna kutoka kwao wanaoshindwa na kupoteza hata pesa za kuhemea kiasi kwamba, wengine wameingia madeni na kulazimika kuuza mali zao ili washiriki na matokeo yake, kubeti au kamari hizo zimewatengenezea umaskini wa makusudi.

Ukweli ni kuwa, asilimia 95 ya wacheza kamari na michezo ya kubahatisha hupoteza fedha zao na hiki ni kiwango kikubwa kuliko wale wanaoshinda.

Soma pia:  Fahamu njia bora za kupanga Fridge 'jokofu' lako

Hasara hiyo huwajeruhi na ‘kuwachanghanya’ sana wao na familia zao. Tunaweza kuambiwa walioshinda ni watu 19 au 20, lakini hatuambiwi waliocheza nchi nzima walikuwa wangapi.

Ni dhahiri kuwa idadi ya washindi ni ndogo mno ukilinganisha na idadi ya washiriki wote.

Ni kweli kuna washindi wenye bahati, ila ‘wanaoliwa” na kulia ni wengi zaidi. Wengine wanasema kushinda hata kwa kiwango cha mamilioni siyo tija, kwani kamari ni ulevi, Hivyo “wewe umeshinda ‘vilaki’ kadhaa, je wengine? Unajua imeleta athari kiasi gani? Kamari ina athari za kisaikolojia za muda mrefu maishani mwako.”

Moja ya athari za kamari ni kumfanya mtu awe tegemezi wa kamari. Matokeo yake ni kupunguza ufanisi na ubunifu katika shughuli za uzalishaji malui.

Kamari inamfanya mtu aamini kwamba ataweza kuyatatua matatizo yake ya kifedha kwa njia ya mkato na kirahisi kwa kucheza kamari. Huu ni ugonjwa wa kisaikolojia; ni kama ugonjwa wa kuwa tegemezi kwa dawa za kulevya.

Suala hili la kamari halikuibuka ghafla pale Ikulu, na hao viongozi wa dini hawakuwa wakitoa hoja mpya. Kwa miaka kadhaa kumezuka makundi ya vijana kugeukia mchezo wa kubahatisha.

Kila kukicha vituo vya kamari ya soka maarufu kama ‘kubeti’ vimekuwa vikiongezeka. Mashabiki wamekuwa wakitumia fedha kwa kubashiri mechi za mpira za mataifa ya nje.

Vituo vya kuchezesha vikachipuka kama uyoga katika maeneo mengi ya Jiji la Dar es Salaam na kwingineko mikoani.

Utafiti kuhusu Kamari

Kamari inavyoliza maelfu

Michezo ya Kamari

Takwimu za Bodi ya Michezo ya Bahati Nasibu, zinaonesha kuwa, mwaka 2017 kwa nchi nzima kulikuwa na vituo vya kubeti 2,684 huku Mkoa wa Dar es Salaam pekee ukiwa na vituo 1,344.

Gazeti moja nchini lilifanya utafiti na kutembelea maeneo ya Mwenge, Magomeni, Kariakoo, Tandale, Tandika, Manzese, Mikocheni, Msasani na Temeke jijini Dar es Salaam na kukuta makundi ya watu wakiwa na makaratasi maarufu kwa jina la ‘mkeka’ huku wakibashiri mechi mbalimbali kwa viwango tofauti vya fedha.

Linamnukuu mmoja wa watendaji wakuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha akisema kuwa michezo hiyo imekuwa chanzo kikubwa cha mapato kwenye bodi hiyo na kuongeza mzunguko wa fedha unaozidi Sh bilioni 1.4 kwa mwezi.

“Huu mchezo umekuwa na mchango mkubwa katika pato la Taifa kwa mwaka 2012/13 hadi Desemba 2015 Sh bilioni 14.0 zilikusanywa na pia kutoa ajira zaidi ya 7,000.”

Soma pia:  Top 10 ya Video zilizoangaliwa mara nyingi Youtube kwa mwaka 2017

Anasema michezo hiyo ya kubahatisha inafanya vizuri, kwani mapato yake kwa bodi hiyo hufikia Sh bilioni 14 kwa mwaka.

Kwa jumla, ipo haja michezo hii ipigwe marufuku kwa kuwa ni kamari; ni haramu kwani ikiachiwa, badala ya tija kwa taifa itazidi kuwa maangamizi; faida zake ni ndogo na zinawafikia wachache, kuliko hasara ambazo ni nyingi na zinalifikia taifa kwa jumla.

Hapa shaka wapo watakaosema hatuwezi kuharibu vizazi vyetu vijavyo kwa sababu kamari inaingiza kodi. Mpaka sasa tumezuia utangazaji tu.

Huenda wahusika wakatafuta njia mbadala ya kuendeleza kamari nchini. Kama tutazuia kamari, hatutakuwa nchi ya kwanza kufanya hivyo.

Kamari nchini Uganda

Nchi jirani ya Uganda imezuia mchezo wa kubeti baada ya Rais Yoweri Museveni kuagiza kuwa mchezo huo upigwe marufuku kwa sababu unawapotosha vijana na kuwafanya waache kufanya kazi.

Serikali ya Uganda imesema haitatoa leseni mpya kwa kampuni za kamari, na kwa wale wenye leseni hawataongezewa muda zitakapomalizika.

Kamari nchini Uingereza

Desemba 2018, Uingereza ilizuia matangazo ya kamari katika mtandao kwa sababu jambo hilo lina madhara kwa watoto na vijana. Wakati mechi za mpira zinapotangazwa mubashara katika runinga watu wengi wamekuwa wakibeti.

Hii ilifika kiwango hatarishi na inakisiwa zaidi ya watu 430,000, wengi wao wakiwa watoto, wameingia mtegoni.

Gazeti moja nchini Uingereza ilifanya utafiti na kuona kuwa wakati kombe la dunia likichezwa kwa muda wa dakika 90 watoto walielemewa na matangazo ya kamari, kiasi kwamba wengi wao walishindwa kujizuia.

Vituo vya kurushia matangazo vilikuwa vikivuna takriban Dola milioni 200 kutokana na matangazo haya. Kampuni za kamari pia zilikuwa zikiingiza mamilioni. Sasa yote haya yamesimamishwa nchini Uingereza.

Kamari marufuku Uingereza, Uganda Tanzania

Repoti ya Gazeti nchini Uingereza kuhusu Kamari Kupigwa marufuku kutangazwa kwnye TV

Kamari Marekani

Nchini Marekani, kamari imekuwa chanzo cha magonjwa. Utafiti uliofanywa mwaka 2012 unadhihirisha kuwa takriban watu milioni sita walikuwa wanahitaji matibabu kutokana na mazoea ya kamari.

Jambo hili limehakikiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) ambalo kwa mara ya kwanza, limeorodhesha kamari kuwa ni chanzo cha ugonjwa wa akili.

Baadhi ya nchi kama Uingereza tayari zimeanzisha kliniki maalum za kuwasaidia watu wenye ugonjwa huu. Daktari Richard Graham ni mtaalamu wa magonjwa haya katika Hospitali ya Nightingale jijini London.

Yeye ameipongeza serikali kwa kutambua janga hili la kamari. Anawatibu wagonjwa 50 kila mwaka ambao maisha yao yameathirika kwa kamari.

Hasara za Kamari

Kamari

Comments

Comments are closed.

More in Makala