Michezo

Serengeti Boys dhidi ya Nigeria AFCON U-17

0
Serengeti Boys Nigeria AFCON
Serengeti Boys

Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana walio chini ya umri wa miaka kumi na saba (2019 AFCON U-17), zinafunguliwa leo saa 10:00 mchana, kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, ambako wenyeji Serengeti Boys wanakata utepe kwa kuumana na Nigeria ‘Golden Eaglets’.

Tanzania inakuwa mwenyeji wa fainali hizo kwa mara ya kwanza, ambako Serengeti Boys inayonolewa na kocha Oscar Mirambo, inawania taji la michuano hiyo, sanjari na kufuzu fainali za Kombe la Dunia la vijana baadaye mwaka huu, malengo ambayo yalikwama katika fainali za mwaka 2017, nchini Gabon.

Jumla ya mataifa nane ya Afrika, yaliyogawanywa katika makundi mawili, yako nchini kupigania ubingwa na nafasi nne za kuiwakilisha Afrika katika fainali za vijana wa umri huo za dunia, zitakazofanyika baadaye mwaka huu nchini Brazil.

Soma pia:  TP - Mazembe yahitimisha safari ya Simba CAF Champion League

Sasa kuelekea ufunguzi wa fainali hizo, mlezi wa Serengeti Boys, Dk. Reginard Mengi, amewaahidi wachezaji wa kikosi hicho pesa taslimu Sh. Milioni 20 kila mmoja, iwapo watashinda mechi mbili kati ya tatu za hatua ya makundi na kufuzu fainali za Dunia.

Tayari Benchi la Ufundi la Serengeti Boys, limejigamba kufanya vizuri kwenye mchezo wa kwanza wa michuano hiyo, ilikopangwa Kundi A la fainali hizo, pamoja na mataifa ya Uganda na Angola, ambazo nazo zitashuka dimbani jioni baada ya Serengeti Boys.

Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo, kesho kwenye Uwanja wa Azam Complex, Kundi B litazindua mechi zake kwa Guinea kumenyana na Cameroon, huku mechi ya pili ikizikutanisha Morocco na Senegal.

Mgeni rasmi katika ufunguzi wa mashindano hayo atakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, ambaye ataambatana na viongozi mbalimbali wa mashirikisho ya soka Tanzania (TFF), Afrika (CAF) na Dunia (FIFA).

Soma pia:  Serengeti Boys dimbani Kesho dhidi ya Uganda

Kuelekea ufunguzi wa leo, kocha wa makipa wa kikosi cha Serengeti Boys, Peter Manyika, jana alisema kuwa kwa mazoezi waliyoyafanya pamoja na maandalizi yaliyofanyika, wana imani wanaibuka na ushindi mbele ya Nigeria.

Manyika alisema kuwa wachezaji wana morali ya hali ya juu kutokana na mafunzo ambayo wamepewa kabla ya michuano ya AFCON, ambako walishiriki michuano ya kualikwa nchini Uturuki ‘Uefa Assist’ na ile ya Rwanda ‘Ferwafa Invitational U-17’ ambako walifanya vema.

“Maandalizi yanakwenda sawa na wachezaji wanatambua kwamba wana kazi kubwa moja tu uwanjani, ambayo ni kutafuta matokeo chanya hakuna jambo lingine zaidi ya hilo.

“Kazi ya mashabiki ni kutoa hamasa hivyo tunaamini uwepo wao uwanjani utatupa nguvu ya kupambana na kufanya kile ambacho wanakihitaji hivyo niwaombe mashabiki watupe sapoti kwa kujitokeza uwanjani,” alisema Manyika.

Comments

Comments are closed.

More in Michezo