Top Stories

Mbaroni kifo cha mwanaharakati

0
Mbaroni kifo cha mwanaharakati
Mwanaharakati Caroline Mwatha

Polisi inawashikilia watu sita wakituhumiwa kuhusika na kifo cha mwanaharakati wa haki za binadamu, Caroline Mwatha. Hata hivyo familia na wanaharakati wenzake wamekanusha kwamba kifo cha ndugu yao kimetokana na kutoa mimba.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI), George Kinoti aliviambia vyombo vya habari vya nchini hapa kwamba mwanaharakati huyo alifariki dunia Februari 6 mwaka huu kwa kutoa mimba katika kliniki moja iliyopo jijini hapa.

Alisema watuhumiwa hao wanahusishwa kwa kusaidia kitendo hicho na kwamba upelelezi wa polisi umebaini alifia kwenye kliniki hiyo Februari 6, kesho yake mwili wake ulihamishiwa katika chumba cha maiti cha jijini hapa.

Alitaja watuhumiwa ni mmiliki wa kliniki hiyo, Betty Akinyi Nyanya maarufu Betty Ramoya, Richard Abudo (ambaye ni mtoto wa Betty), Georgia Achieng, Michael Onchiri maarufu Dk Mike, Alexander Gikonya (anayedaiwa kuwa rafiki wa kiume wa mwanaharakati huyo) na dereva wa teksi, Stephen Maina.

Soma pia:  Mashua ya plastiki ya Kenya kufanya safari ya kihistoria

Kinoti alitaja namba za usajili za gari lililosafirisha mwili wa mwanaharakati huyo hadi kwenye chumba cha maiti na kusema kwamba awali jina lake lilitambulika kama Carol Mbeki na siyo Caroline Mwatha.

“Februari 6, 2019, Caroline alikwenda kliniki ijulikanayo kwa jina la New Njiru Community Centre iliyopo Dandora Phase 1.

Inaaminika mchakato wa kutoa mimba ulisimamiwa na mmiliki wa kliniki hiyo aitwaye Betty Akinyi Nyanya maarufu kama Betty Ramoya na mwingine anadaiwa ni daktari, Michael Onchiri au Dk Mike,” ilisema taarifa hiyo ya DCI.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo wa upelelezi wa jinai, kabla ya kifo chake, Mwatha alifanya mawasiliano na Gitau, anayefanya kazi Isiolo ambaye inasemekana ni rafiki yake wa kiume.

Soma pia:  10 kortini kwa kufanyakazi bila vibali

Alisema mawasiliano yao yalihusu nia ya kutoa mimba hiyo ya miezi mitano. DCI Kinoti aliongeza kwamba, daktari ambaye hakutajwa jina lake, inadaiwa alitakiwa kufanya mchakato huo wa kutoa mimba kwa Sh 7,000 lakini alipunguza ikawa Sh 6,000 baada ya kuombwa afanye hivyo.

Alisema kiasi hicho cha fedha inadaiwa kilitumwa na rafiki huyo anayedaiwa kuwa rafiki yake wa kiume.

Familia imekanusha taarifa hiyo ya polisi na kusema ndugu yao alikutwa mwili wake umekatwa kwenye paja na shingo na kitu kikali . Familia yake ilihoji ikisema tangu awali walikwenda kutafuta kwenye chumba cha maiti na hawakukuta mwili wa ndugu yao.

Comments

Comments are closed.

More in Top Stories