Top Stories

Uzalishaji dhahabu Sudan wafikia tani 93

0
Uzalishaji dhahabu Sudan
Uzalishaji dhahabu Sudan

Wizara ya Madini nchini Sudan imesema kuwa uzalishaji wa dhahabu umefikia tani 93 katika mwaka ulioisha wa 2018, ambayo thamani yake ni sawa na dola za Marekani bilioni nne.

Mkurugenzi wa Shirika la Utafiti wa Kijiolojia (GRC), Mohamed Abu Fatima, alisema Wizara ya Madini inakabiliwa na changamoto ya kuanzisha njia na sera za kusimamia mauzo ya dhahabu kikamilifu ili kufikia mapato ya dola za Marekani bilioni tatu.

Abu Fatima alisema kuwa kuna haja ya kuwa na kampuni kubwa za uchimbaji wa dhahabu pamoja na kukamilisha miundombinu muhimu, ikiwemo maabara pamoja na uanzishwaji wa masoko ya dhahabu.

Imeelezwa kuwa Shirika la Utafiti wa Kijiolojia (GRC) ni mkono wa kiufundi wa Wizara ya Madini. Hata hivyo, wizara hiyo haikuweka wazi kiwango halisi cha dhahabu kilichouzwa nje ya nchi pamoja na mapato yaliyopatikana mwaka jana.

Soma pia:  Sudan kufunga mipaka yake na Eritrea

Pamoja na mafanikio hayo, wizara hiyo ya madini ilisema kuwa katika kipindi cha nusu ya mwaka 2018, kulikuwa na magendo ya dhahabu tani 48.8.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, kiwango cha dhahabu kilichozalishwa katika kipindi cha nusu ya mwaka jana kilifikia tani 63.3, huku Benki Kuu ya Sudan (CBoS) iliweza kununua asilimia 10 tu ya dhahabu yote iliyozalishwa.

Hata hivyo haikuelezwa wazi kama tani hizo 48.8 zilikuwa zimeuzwa kimagendo au zilifichwa na wachimbaji wadogo na kampuni za uchimbaji ili serikali isiweze kuzipata.

Imeelezwa kuwa dhahabu ni chanzo kikuu cha fedha za kigeni nchini humo hasa baada ya Sudan Kusini kujitenga ambako theluthi mbili ya hifadhi yake ya mafuta ilikuwa huko.

Taarifa zinasema kuwa katazo la matumizi ya fedha za kigeni lililowekwa na Benki Kuu nchini humo limekuwa kikwazo kwa maendeleo ya sekta ya madini, lakini pia linasababisha wachimbaji wadogo kuuza madini yao kimagendo nchi jirani.

Soma pia:  UN yasaidia Sudan Kusini kujikinga na ebola

Sudan imetajwa kuwa ya tatu kwa uzalishaji wa dhahabu ikitanguliwa na Afrika Kusini na Ghana. Maofisa nchini humo walisema kuwa wanatarajia kuongeza uzalishaji wa dhahabu hadi ufikie tani 140.

Comments

Comments are closed.

More in Top Stories