Top Stories

Unywaji kahawa ukihimizwa utaongeza soko la ndani

0
Unywaji kahawa ukihimizwa utaongeza soko la ndani
Kahawa

Leo umekunywa kahawa au chai? Basi fahamu unapokwenda dukani kununua kahawa na kisha kutumia kinywaji hicho, unachangia kuwainua wakulima nchini wasitegemee zaidi soko la nje.

Mwezi Januari mwaka huu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitembelea Mkoa wa Ruvuma kwa ziara ya siku sita. Miongoni mwa mambo aliyohimiza, ni unywaji kahawa.

Katika ziara hiyo, Majaliwa alitembelea Halmashauri za Mbinga, Nyasa, na baadaye anahitimisha katika Manispaa ya Songea kwa kuwahutubia wananchi katika Uwanja wa Majimaji.

Pamoja na mambo mengine, Majaliwa anazindua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo kuweka jiwe la msingi la jengo la Tanesco Songea na kuzindua ujenzi wa Barabara ya Mbinga – Mbamba Bay kwa kiwango cha lami yenye urefu wakilomita 66.

Barabara hiyo inajengwa na Kampuni ya CHICCO kutoka China. Akiwa wilayani Mbinga, baada ya kuwahutubia wananchi katika viwanja vya Unyoni nje kidogo ya mji huo, Waziri Mkuu aliendesha kikao kilichohusisha wadau wa zao la kahawa.

Yapo masuala mengi yaliyojiri katika kikao hicho ambacho madhumuni yake yalikuwa kuwaleta pamoja wadau wa zao hilo ili kutoa mawazo yao katika kuinua uzalishaji na kukuza uchumi wa wakulima, wafanyabiashara na kukuza pato la taifa kwa jumla.

Ukiacha taasisi za kifedha kama Benki za CRDB, NMB na TPB, Taasisi ya Utafiti ya zao la Kahawa (TaCRI) ilikuwa miongoni mwa wadau muhimu walioshiriki katika kikao hicho.

Ndani ya kikao, baadhi ya wakulima walionesha uhitaji mkubwa wa kupanda miche zaidi ya kahawa kwa maana ya miche inayozalishwa kwa kiasi kikubwa na TaCRI na pia suala la soko lilizungumziwa kwa kina. Waziri Mkuu anahimiza kila mdau wa zao la kahawa kufanya kila linalowezakana ili afurahie kazi yake.

Anawaagiza maofisa ugani kuhakikisha wanakwenda katika mashamba kuwasaidia wakulima vijijini, badala ya kucheza na kompyuta ofisini.

Anaagiza pia vyama vyote vya msingi kuunda vyama vya ushirika vya wakulima (AMCOS) mpya na uongozi mpya wenye utaratibu mpya na kisha kufanya usajili upya.

Sambamba na hilo akasema ni muhimu orodha ya wakulima ikawapo kwa maana ya kujua nani ana shamba la kahawa la ukubwa gani na lipo eneo gani, ili takwimu hizo ziisaidie serikali kuleta mbolea kwa idadi sahihi.

Waziri Mkuu anafafanua kuwa, msimu ujao kahawa hazitapelekwa tena kwenye mnada Moshi kutokana na mikanganyiko iliyokuwepo huko nyuma (ambayo imeshashughulikiwa na serikali) na badala yake sasa, Mbinga itakuwa makao makuu ya kanda ya kusini katika ununuzi wa kahawa.

Majaliwa anataja kanda nyingine zitakazotumika kununua kahawa kuwa ni pamoja na Songwe na Mbozi katika ukanda huo na kwamba kazi hiyo itasimamiwa kwa karibu na Bodi ya Kahawa inayotakiwa kuhakikisha utekelezaji wake unafanyika vizuri na kwa wakati.

Waziri Mkuu pia anaishauri Kampuniya Aviv Tanzania Limited iliopo wilaya ya Songea yenye shamba lake lenye ukubwa wa hekta 1,990 kuendelea kushirikiana na TaCRI katika kuongeza uzalishaji wa miche.

“Nimejulishwa kuwa Aviv Tanzania Limited hawalimi tu kahawa, lakini pia wanatafuta masoko na wanauza kahawa yao katika soko la kimataifa. Kwa nini sisi wengine tusijifiche nyuma yake ili watuonyeshe masoko hayo?” Anahoji Majaliwa.

Waziri Mkuu anaagiza pia kila halmashauri mkoani Ruvuma kuwa na shamba la miche ya kahawa takribani 200,000 kwa ajili ya mbegu na kuigawa kwa wakulima bure katika msimu wa kilimo ujao ili kuongeza tija.

“Jingine nimalize na ninyi watumishi wenzangu, huko maofisini, hasa hapa Ruvuma anzeni kunywa kahawa badala ya chai ili kuhamasisha wengine kunywa na kununua kahawa ili kukuza uchumi,” anasema.

Akitoa mchango wake katika kikao hicho, Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa TaCRI, Dk Deusdedit Kilambo anasema TaCRI iko tayari kutoa mafunzo katika ngazi ya vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS) yahusiyo kilimo bora cha zao hilo ili kuinua zaidi kilimo cha kahawa.

Anasema TaCRI inafanya kazi kwa karibu sana na AMCOS mbalimbali nchini, na kwamba hivi karibuni, waliwapa AMCOS ya Manushi iliyoko Moshi Vijijini miche ya mbegu bure kama sehemu ya kutoa hamasa kwa wakulima wa kahawa.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji Mkuu huyo, TaCRI imejipanga kukidhi mahitaji ya miche ya kahawa kitaifa, kwa kushiriki katika uzalishaji miche milioni sita hadi saba kwa mwaka kwa ajili ya vyama vya msingi, watu binafsi na taasisi zisizo rasmi.

Anasema changamoto ya bungua mweupe iliyosumbua katika sekta ya kilimo cha kahawa kwa muda mrefu, inaelekea kupata ufumbuzi wa kudumu hasa baada ya dawa aina ya DDT iliyokuwa ikitumika awali kuondolewa sokoni.

Akifafanua, Kilambo anasema, TaCRI imetafiti na kugundua dawa mpya aina ya Fiproni l inaweza kuwa mwarobaini wa mdudu huyo lakini dawa hiyo inasubiri kibali kutoka taasisi inayoshughulikia viuatilifu ya TPRI ili dawa hiyo kuruhusiwa kuanza kutumika.

Akizungumza na mimi muda mfupi baada ya kumalizika kikao hicho, Kilambo anasema vikao kama hivyo ni umuhimu kwani, pamoja na mambo mengine, vinasaidia watu kukumbushwa majukumu, kupokea maagizo na mawazo mapya pamoja na kujitathmini katika utekelezaji.

Anasema wakati juhudi zinafanyika ili kuboresha zaidi kilimo cha kahawa, zinapaswa kwenda sambamba na kuhamasisha jamii kupenda kunywa kahawa.

“Jukumu kubwa ambalo wote tunatakiwa kulifanya muda mwingi katika maisha yetu ya kila siku, ni kuhamasisha na kufungua sehemu za biashara ya unywaji wa kahawa. Anasema Kilambo.”

Anasema unywaji kahawa ukiwa mkubwa nchini, utasaidia kuongeza soko la ndani la zao hilo badala ya kutegemea soko la nje.

Akizungumzia masuala ambayo wanakwenda kuyashughulikia baada ya kikao hicho, Mkurugenzi huyo anayataja kuwa ni kujipanga kuzalishaji miche mingi zaidi, kutoa mafunzo kwa wakulima na wagani, yote yakilenga kuendesha kilimo cha kahawa kibiashara.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme akifafanua jambo katika kikao hicho anasema, mazao ya kimkakati mkoa wa Ruvuma ni pamoja na kahawa, korosho na mahindi.

Hata hivyo, anasema kahawa ndilo zao linalochangia sehemu kubwa ya mapato kuanzia ngazi ya familia hadi mkoa.

Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa, zaidi ya kilo milioni 20 za kahawa zilivunwa katika msimu wa kilimo kwa mwaka na kwamba, viwanda vya kuongezea thamani zao hilo mkoani humo vipo vinne mkoani; wilaya ya Mbinga vipo vitatu na kimoja kipo wilaya ya Songea

Comments

Comments are closed.

More in Top Stories