Top Stories

Kagera Sugar iliwekeza Tanzania

0
Kagera Sugar iliwekeza Tanzania
Dk. Ashatu Kijaji

Serikali imeeleza kuwa kiasi chote cha dola za Marekani millioni 65 zilizokopwa na Kiwanda cha Sukari cha Kagera kutoka Benki ya CRDB kwa udhamini wa Serikali mwaka 2004 kimewekeza nchini hakijapelekwa kuwekeza katika nchi ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Hayo yalielezwa bungeni hapa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji (Pichani) wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Rufiji Mohammed Omary Mchengerwa, aliyetaka kujua sababu za Serikali kumdhamini mwekezaji wa Kiwanda hicho kukopa kiasi hicho cha fedha ambacho kimepelekwa kuwekezwa nchini Kongo wakati Tanzania ina Uhaba wa Sukari.

Akijibu, Dk. Kijaji alisema kuwa uwekezaji uliofanywa katika Kiwanda cha Kagera ni takribani dola za Marekani millioni 250 hivyo haiwezekani mwekezaji kukopa millioni 65 na kuzipeleka DRC ili hali kiwango cha uwekezaji nchini ni kikubwa.

“Mwekezaji wa Kiwanda hicho ni wa ndani amejitahidi kuajiri Watanzania wengi hivyo Serikali ipo katika mchakato wa kukiwezesha kiwe cha mfano ili kiendelee kuleta matokeo chanya kwa Watanzania”. alisema Dk Kijaji.

Katika swali la Mbunge huyo alitaka kujua kiwango cha hisa ambacho Serikali inamiliki katika kiwanda cha Sukari cha KAgera na kiasi cha fedha kilichokopwa na kulipwa na mwekezaji huyo kupitia udhamini huo wa Serikali.

Dk. Kijaji alieleza kuwa Serikali kwa sasa haimiliki hisa zozote katika Kiwanda hicho na akaongeza kuwa hisa zake katika kiwanda hicho ziliuzwa mwaka 2001 baada ya kukibinafsisha kwa Kampuni ya Kagera Saw Mills Limited.

Aidha, Dk. Kijaji alifafanua kuwa mwekezaji wa Kiwanda hicho alikopa kiasi cha dola za Marekani millioni 65 kwa kutumia udhamini wa Serikali mwaka 2004, ikiwa ni udhamini (guarantee) kwa kipindi cha miaka 12.

Alisema kuwa mpaka sasa Kiwanda hicho kimerejesha zaidi ya dola za Marekani millioni 56.88, sawa na asilimia 87.5 ya mkopo wote, na kwamba marejesho ya mkopo uliobaki wa dola millioni 8.12 yatafikia ukomo wake Julai, 2019.

Comments

Comments are closed.

More in Top Stories