Burudani

Jose Ability kufuata nyayo za Diamond Platnumz

0
Jose Ability kufuata nyayo za Diamond Platnumz
Jose Ability

Mafanikio anayopata nyota Nassib Abdul ‘Diamond Platnumz’ ni mfano wa kutosha kwa wengine hadi wanatamani kuyafi kia ili kufanya vizuri katika muziki wa kizazi kipya.

Miongoni mwa wasanii wanaokubali kile anachokifanya Diamond, ni Joseph Nyallasha au ‘Joseability’ na kuamini kuwa huenda siku moja akafanya naye kazi.

Katika mahojiano, msanii huyo aliyekuja kutambulisha sanaa yake, alisema Diamond ni msanii wa kimataifa ambaye licha ya kuwa na kipaji, anajua kufanya biashara.

Jose anasema kuna mwanamuziki na mfanyabiashara huku akimweka Diamond kuwa ni mfanyabiashara hivyo, hana budi kupambana kufikia hatua ya maendeleo kama yake.

Kingine anatamani kufanya kazi na msanii huyo akiamini anaweza kumsaidia kufikia malengo ya kuufanya muziki wake kuwa biashara kubwa itakayomlipa.

Anasema kuna wasanii wengi wenye vipaji lakini hawajui namna ya kuufanya muziki kuwa biashara. Lakini kwa Diamond anajua anachokifanya. “Natamani sana kupata msaada wa Diamond, najua nikifanya naye kazi nitafika mbali, nimeshuhudia kwa kuona wengine namna wamefanikiwa kupitia yeye,”anasema.

Jose Ability ni Nani?

Huyu ni msanii mchanga anayekuja kwa kasi katika muziki akitokea Mwanza alikozaliwa. Ni mtoto wa tano katika familia ya watoto sita ya Mzee John Nyallasha.

Alianza muziki 2011 ingawa rasmi ilikuwa ni mwaka 2016 kutokana na kubanwa na masomo ya chuo, alikokuwa anachukua shahada ya uandishi wa habari mkoani Arusha. Na sasa amemaliza masomo na kurudi baada ya kuachia wimbo wake mkali mwishoni mwa mwaka jana unaofahamika kama Sweat Love.

Soma pia:  Mashabiki wamtibua Davido
https://www.youtube.com/watch?v=4sRtyu3f2-w
Jose Ability

Wimbo huo hakika umeanza kufanya vizuri ingawa bado anahitaji mashabiki wa muziki kumuunga mkono kufikia kile anachokiota kwa kufikisha muziki huo mbali zaidi.

Anasema sio kwamba huo ulikuwa ni muziki wake wa kwanza bali wa pili kwani wa kwanza aliutoa mwaka 2011 ukifahamika kwa jina la Umenitupa na pia, aliwahi kushirikishwa na wasanii mbalimbali.

“Nashukuru tangu nimeachia wimbo wangu wa Sweet Love umeanza kufanya vizuri na taratibu watu wameanza kuupokea, lakini bado nahitaji sapoti kubwa kuyafikia mafanikio,”anasema.

Safari yake ya Muziki

“Muziki ni ajira, napenda kuimba nikiamini itanisaidia kusonga mbele kimaisha,” anasema. Anasema anaamini atafika kama atapata watu wa kumuunga mkono kwani anajua akiwa mwanamuziki mchanga kuna changamoto nyingi ni lazima upate watu wa kukuongoza.

“Unajua kwa sasa nasimamiwa na baba yangu mdogo, namshukuru sana kwa kupenda kile ninachokifanya, amekuwa akinisaidia na anatamani kuona napata mafanikio,”anasema.

Anasema baba yake huyo anayefahamika kama Amosi Nyallasha amekuwa ni msaada na humsimamia kwa sasa hadi pale atakapopata msimamizi mkuu atakayemuongoza njia ya kupita kibiashara na kufahamika zaidi.

Soma pia:  Ray C kuolewa na mzungu Uingereza

Aliyemvutia kuanza kuimba

Anasema kuna wasanii wengi wanamvutia lakini zaidi ni Elias Barnaba maarufu Barnaba na anapenda anavyoimba mashairi mazuri yanayogusa watu.

Kingine anasema msanii huyo muziki wake haufi, kila siku ukisikiliza una ladha isiyochosha. Pia, anasema sio msanii wa mambo mengi, anaishi maisha ya kawaida ambayo wengine wanaishi.

Barnaba ni miongoni mwa wasanii anaotamani kufanya nao kazi na anasema anatarajia ndani ya mwaka huu kukutana naye kuweka mipango.

Anasema huko nyuma aliwahi kuwasiliana naye na akampa nafasi ya kuonana lakini hakuweza kutokea kutokana na kubanwa kimasomo.

Changamoto anazopitia

Anasema vyombo vya habari hasa televisheni vimekuwa vikimpa wakati mgumu kumuunga mkono kwani anapopeleka wimbo wake haupewi kipaumbele.

Hata anapofuatilia haoni ukipigwa jambo ambalo kuna wakati limekuwa likimkatisha tamaa. Anasema hataki kukata tamaa mapema bali anajipanga kupambana akiamini siku moja mambo yatakuwa mazuri na kupokelewa kama ilivyo kwa wengine waliowahi kutoka na kufanikiwa.

Changamoto nyingine anasema muziki unatumia nguvu nyingi kutoa bila kuwa na uhakika wa kurudisha. Anatolea mfano kuwa katika wimbo wake wa Sweatlove ametumia zaidi ya Sh 500,000 ila hajaanza kurudisha.

Soma pia:  Mr. P - My Way (Official Music Video)

Amekuwa akipata shoo za kujitolea kanda ya ziwa na kwenda kuzifanya bure ili kujitangaza. Pia, aliwahi kutumbuiza mkoani Arusha katika moja ya matamasha na shughuli za kumtafuta Miss Arusha.

Kwa upande wa soko, anasema ni kugumu kwa sababu kuna ushindani mkubwa kila mtu anapambana kuachia ngoma kali itayovutia kibiashara.

Mipango yake kwa sasa

Anasema baada ya Sweetlove anatarajia kuachia nyimbo nyingine mfululizo kuanzia mwezi huu.

“Natarajia ndani ya mwezi huu nitaachia kisha nyingine itafuata April, lengo ni kuendelea kuwapa mashabiki zangu muziki mzuri usiochosha kusikiliza,”anasema.

Anachokichukia katika tasnia ya Muziki Tanzania

Anasema wasanii wengi wakubwa hawapendi kuwaunga mkono chipukizi wala hawaoni umuhimu.

Jose Ability anasema kuna haja kubwa ya wasanii hao kuwasaidia hasa pale wanapohitaji msaada kutoka kwao. Kingine anasema watoe nafasi ya kuwasikiliza na kuona vipaji vyao kabla ya kuwakatisha tamaa.

Baba yake mdogo Jose, Amos Nyallasha anasema anamuamini kijana wake ana uwezo iwapo atapata watu wa kumsaidia kutimiza malengo yake hawatajuta.

“Natamani kumuona Jose kwenye mafanikio na siku zote nimekuwa nikimuunga mkono kutimiza malengo yake,”alisema na kuwaomba mashabiki wa muziki kumuunga mkono kijana wake ili aweze kufahamika ndani na nje ya nchi.

Comments

Comments are closed.

More in Burudani